Ni masikitiko makubwa kwamba mtoto mwenye ulemavu wa ngozi
katika Kijiji cha Kipeta, Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa amejeruhiwa
na watu wasiojulikana baada ya kukatwa kiganja cha mkono wa kulia.
Tukio hilo limekuja kipindi ambacho Serikali
imeweka mikakati ya kupambana na wauaji wa albino nchi nzima. Pia, tukio
hilo limekuja siku chache tu baada ya wananchi wenye ulemavu wa ngozi
kumfikishia kilio chao Rais Jakaya Kikwete ambaye aliwaahidi kuwa
serikali yake itahakikisha inawalinda na kuwatafuta watu wanaojihusisha
na kukata viungo vyao au kuwaua.
Pamoja na hatua hiyo ya Rais Kikwete wiki
iliyopita, watu wenye imani potofu za kishirikina mwishoni mwa wiki
walimkata kiungo mtoto huyo baada ya kumpiga mama yake na kitu kizito
hadi akazirai. Tunaambiwa kwamba alipozinduka alipiga kelele kuomba
msaada kutoka kwa majirani. Hata hivyo, alipata msaada baada ya watu hao
kukimbia, huku tayari wakiwa wametekeleza uovu wao. Kama wananchi wengi
wanavyofahamu, huo ulikuwa ni mwendelezo wa matukio mengi kama hayo
dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino.
Tumepata faraja kusikia kwamba Serikali tayari
imewakamata washukiwa kadhaa wa tukio hilo sawa na wale waliofanya uovu
kama huo mwezi uliopita katika Kijiji cha Shilabela, mkoani Geita ambako
watu kadhaa walivamia nyumba ya mama mmoja na kumpora mtoto wake
albino, huku wakimjeruhi vibaya mama huyo alipokuwa akipambana nao
kujaribu kumwokoa mwanaye.
Tunaweza kuorodhesha matukio mengi ya albino
kuuawa au kujeruhiwa, lakini tunadhani kwamba pengine wakati umefika
sasa kwa jamii kuelekeza nguvu zake katika kukomesha imani hizo potofu,
kwani ni dhahiri kwamba sheria kali pekee zimeshindwa kukomesha vitendo
hivyo vya kinyama dhidi ya albino.
Hakuna sababu za kisayansi zinazotolewa kuhusu
kazi za viungo vya albino, ingawa kila likifanyika tukio la aina hiyo,
jamii huambiwa ni kwa shughuli za ushirikina; kwamba watu wanaotafuta
utajiri kwa njia za mkato ndio wanaohusika.
Kwamba waganga wa kienyeji ambao hufanya shughuli
zao kwa kupiga ramli ndio huwaagiza wateja wao kupeleka viungo vya
albino ili watengenezewe mambo yao. Ni kutokana na hali hiyo Serikali
imeamua kupiga marufuku upigaji ramli na katika maeneo mengine nchini
wapigaji ramli wamekamatwa ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Tunaipongeza Serikali kwa hatua hiyo, lakini
tunadhani iko haja kwake na jamii kwa jumla kushughulikia watu
wanaokwenda kwa wapiga ramli wakijidanganya kwamba watatajirika au
kupata vyeo kwa imani hizo potofu. Ni bahati mbaya kwamba baadhi ya
wanasiasa ambao wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupiga vita upigaji ramli
unaodaiwa kuwa chanzo cha mauaji ya albino ndio wanaokwenda kupiga
ramli na huenda ndio wanaowatuma wengine kufanya hivyo kwa malipo
kidogo.
Katika mapambano dhidi ya ushirikina ni vyema
Serikali, asasi za kiraia na jamii kwa jumla vikatoa elimu ili kila
mwananchi atambue kwamba siri ya utajiri ni kufanya kazi kwa juhudi na
weledi ofisini, mashambani, migodini na kwingineko. Vilevile, watu
wapewe elimu ya kujitegemea kuhusu namna ya kupata mitaji, kuweka
kumbukumbu na kujiepusha kufanya anasa na matumizi yasiyo na maana. Hiyo
ndiyo siri pekee ya mafanikio na wala siyo viungo vya albino.
0 Comments