Sumaye aziasa nchi Afrika kuwekeza katika ushirikiano.

Tokeo la picha la sumae aanzisha
HeWaziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye (pichani) , ameziasa nchi za kiafrika ikiwamo Tanzania, kuwekeza katika ushirikiano miongoni mwao na kuyatumia masoko yaliyopo ndani ya ukanda huo badala ya nje yenye ushindani mkubwa. Sumaye aliyasem yea hayo juzi kwenye mkutano wa 12 wa mwaka wa uchumi barani Afrika uliofanyika kwenye Chuo cha Sheria cha Columbia kilichopo jijini New York, Marekani na hotuba yake kupatikana kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam. Sumaye alisema mgawanyo wa bara la Afrika uliofanywa na wakoloni, ulidhoofisha uchumi wa mataifa ya bara hilo na kuyafanya kuwa tegemezi kwa ‘mabwana wakubwa’ na udhaifu uliotokana na uwezo mdogo. “Ili kukabiliana na changamoto hiyo, nchi za Afrika lazima zianzishe kanda zenye nguvu kiuchumi na ambapo biashara zitafanyika. Lazima nchi hizo zikubali kwamba kutengana kunachagiza udhaifu,” alisema. Pia alisema sekta binafsi inapaswa kulindwe na ipewe umuhimu unaostahili na viwanda vichanga vilindwe na serikali. Kwa mujibu wa Sumaye, sera za uwekezaji zinapaswa kupitiwa upya ili ziwalinde wawekezaji, maslahi ya nchi na ya umma kwa vile baadhi ya hizi (sera) zimetokana na ushawishi wa ‘wakubwa’. Alisema nchi zilizoendelea ama mawakala wao wanaingilia utungwaji wa sera za uwekezaji kupitia ushauri ama kufadhili fedha na kutoa mfano wa ripoti ya Oxfam ya mwaka jana kuhusu utajiri wa dunia. “Ninadhani tunapaswa kuziangalia upya hizi sera ili wawekezaji wanufaike, nchi inufaike na raia wanufaike,” alisema. Sumaye alisema jitihada za kukuza uchumi wa nchi na kuongeza kipato kwa raia, mikakati madhubuti inatakiwa kufikiwa ili kuwapo usindikaji wa mazao ya kilimo na uongezaji thamani kwa rasilimali nyingine za nchi. ‘’ Wanaoshiriki kuongeza thamani ya mazao na rasilimali zinazotoka Afrika wataendelea kuwa matajiri na Afrika itabaki kuwa masikini. Serikali za Afrika na sekta binafsi lazima wapitie upya hali hii ili kufanikisha azma ya kuuza kwenye Soko la Dunia bidhaa zilizosindikwa. Sumaye, alizungumzia pia sekta ya elimu akihimiza wasomi kuwa na uzalendo utakaowafanya kuzitumikia nchi zao na kuzisaidia kuondokana umasikini na uchumi mbovu. “Elimu inamfanya mtu kuwa huru, kuwa na hulka ya kuhoji, uimara wa kukabiliana na changamoto na kuzitambua fursa zilizopo kwenye mazingira yake na kutumia rasilimali asilia kwa manufaa yake,” alisema. Alisema kupitia elimu bora, Afrika inahitaji mabadiliko ya kweli ya kifikra, namna ya kutenda, uendeshaji uchumi na mifumo ya siasa ili vichagize maendeleo ya haraka yanayohitajika barani humo. “Barani Afrika ikiwamo nchini kwangu, hatujafikia mabadiliko halisi. Waafrika tunatakiwa kubadilika kwa namna ya kufikiri, kufanya kazi, kutumia na kuwekeza,” aliyeaa.

Post a Comment

0 Comments