ISIHAKA ; UMRI TATIZO YANGA

Tokeo la picha la YANGA
Dar es Salaam. Nahodha wa Simba, Hassan Isihaka amesema kinachowasumbua sasa Yanga ni umri wa wachezaji wao.
Simba iliifunga Yanga bao 1- 0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Isihaka aliiambia Mwananchi kuwa kikosi cha Simba kina wachezaji wengi vijana kuliko Yanga ndio maana wanaonyesha kiwango bora uwanjani kuliko wapinzani wao.
Alisema kila mmoja aliona jinsi Simba ilivyotawala mchezo kutokana na kuwa na damu changa ambazo zilisababisha wakacheza soka la kasi na pasi nyingi.
“Tunafurahi na watu lazima wajue mpira ni magoli na burudani, hivyo tunaamini tumewaburudisha mashabiki wetu kwa soka safi tulilocheza, kila mtu aliona tulikuwa bora kuliko wapinzani wetu Yanga.
“Kinachotusaidia sisi tukawa bora uwanjani ni aina ya wachezaji tuliopo katika timu yetu, wengi ni vijana na ndio kwanza timu inajengwa hivi sasa kupitia damu changa tofauti na Yanga wachezaji wao wengi na wamekaa na timu muda mrefu, hivyo watasubiri sana kwetu,” alisema Isihaka.
Hata hivyo Isihaka aliwataka wenzake kuendelea kupambana katika michezo mingine ijayo na ushindi huo usiwafanye wakaridhika mapema bali uwe chachu ya kufanya vizuri kwa mechi nyingine.
“Bado tuna safari ndefu, sawa tumepata ushindi lakini hatupaswi kuridhika, tunahitaji kupambana zaidi, tunatakiwa kushinda michezo mingine yote iliyobaki, kwani ligi ya msimu huu ni ngumu sana.
“Ushindi dhidi ya Yanga uwe chachu ya kufanya vizuri katika mechi zinazokuja, ni ushindi ambao umerudisha morali ya timu na umetupa furaha pia hivyo tunatakiwa kujituma , kupambana na kumaliza tukiwa katika nafasi mbili za juu kwani hao waliotangulia wanaweza kupoteza hivyo hatupaswi kukata tamaa,” alisema Isihaka.
Kwa ufupi
Simba iliifunga Yanga bao 1- 0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments